WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Jumuiya ya Madola inaweza kuiga mbinu
ambazo Tanzania imetumia katika kupambana na rushwa zikiwemo za
kujumuisha wadau tofauti kwenye vita hiyo.
Ametoa
kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa
Jumuiya ya Madola, Bibi Patricia Scotland walipokutana kwenye mkutano wa
kimataifa uliojadili jinsi ya kupambana na rushwa duniani uliofanyika
Lancaster House, jijini London, Uingereza.
“Tanzania
iko tayari kushirikiana na ninyi katika kujenga timu hii na ili uweze
kupata picha halisi, nakukaribisha Tanzania uje ujionee hatua ambazo
tumechukua hadi kufikia hapa tulipo kwenye vita hii dhidi ya rushwa,” alisema Waziri Mkuu ambaye alihudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Alimweleza
Katibu Mkuu huyo kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kupambana
na rushwa kutokana na ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka kwa
wananchi.
“Wananchi
wanafurahia juhudi za Serikali, vyama vya kiraia pia vinaunga mkono
jitihada zetu na vyombo vya habari vinashirikiana nasi katika vita hii,”
alisema.
Waziri
Mkuu alitoa wito huo baada ya kuelezwa na Bibi Scotland kwamba anataka
kuanzisha idara malum kwenye Jumuiya hiyo ambayo itasimamia mapambano
dhidi ya rushwa na makosa ya jinai.
“Nataka
tuwe na idara yenye watu mahiri wa idara za uhasibu, mahakama yenyewe
ikiwemo waendesha mashtaka na wanasheria kutoka kwenye nchi kadhaa ili
washirikishane uzoefu kutoka kwenye nchi zao. Ninaamini katika nchi 53
ambazo ni wanachama wetu, sitakosa watu wa aina hii,” alisema.
Alisema
ameamua kufanya hivyo ili aweze kuendanana na malengo makuu matatu ya
jumuiya hiyo ambayo ni kupiga vita rushwa, kuhimiza utawala bora na
usimamizi wa demokrasia.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, MEI 14, 2016.
0 comments:
Post a Comment