MBUNGE wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi akizindua
gari la kubeba wagonjwa (ambulance)
|
MBUNGE wa Mafinga Mjini, Cosato
Chumi kwa kushirikiana na asasi ya kimataifa ya Rafiki Surgical Mission
ya Australia ametoa msaada wa gari la kubeba wagonjwa (ambulance) kwa
ajili ya matumizi ya hospitali ya wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa
iliyopo katika jimbo lake hilo.
Gari hilo aina ya Toyota Hiace
lenye thamani ya Sh Milioni 40 lilikabidhiwa jana kwa uongozi wa
halmashauri ya mji wa Mafinga inayosimamia uendeshaji wa hospitali hiyo
katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mashujaa,
mjini Mafinga.
Akikabidhi msaada huo Chumi
alisema; “napenda ifahamike kwamba gari hilo limenunuliwa na asasi hiyo
ambayo mimi ni rafiki yao mkubwa. Uadilifu na uaminifu kwa taasisi hiyo
umetufanya tushirikiane vyema katika mambo mengi kwa faida ya wananchi
wa jimbo langu la Mafinga.”
Alisema gari hilo la wagonjwa
ni rafiki kwa wagonjwa na wajawazito kwa kuwa lina vifaa tiba
vinavyoweza kutumika kutolea huduma wakati wakipelekwa hospitalini.
Baada ya kukabidhi gari hilo,
Chumi ambaye ni mbunge wa kwanza wa jimbo hilo jipya, mkoani Iringa
alikumbusha vipaumbele vyake kwa wapiga kura wake kuwa ni kuhakikisha
linapata huduma bora ya maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara.
Akishukuru kwa msaada huo,
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Dk Innocent Mhagama
alisema kabla ya msaada huo, hospitali hiyo ya wilaya ilikuwa na gari
moja tu la kubeba wagonjwa.
“Pamoja na kuhudumia hospitali
hiyo ya wilaya, gari hilo moja lilikuwa likihudumia vituo vingine 18 vya
kutolea huduma katika wilaya hiyo hivyo,” alisema.
Alisema kupatikana kwa gari
hilo jipya kutasaidia kuboresha huduma hiyo kwa kuokoa maisha ya
wagonjwa na maisha ya mama na mtoto ambayo ni kipaumbele katika utoaji
wa huduma za afya.
Akizungumzia huduma ya mama na
mtoto katika hospitali hiyo ya wilaya, Dk Mhagama alisema kwa wastani
wajawazito 500 wanajifunga kila mwezi hospitalini hapo.
“Kati yao wajawazito zaidi ya
100 huwa wanapata huduma za dharula huku wastani wa wajawazito 10
wakipatiwa huduma za rufaa,” alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji
wa Mafinga, Charles Makoga alisema halmashauri yake kwa kushirikiana na
mbunge huyo itahakikisha inatekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na
Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk John Magufuli, mbunge na madiwani ili
kuboresha huduma kwa watu wake.
0 comments:
Post a Comment